Katika kupekuapekua makabrasha yangu wiki hii, nimekutana na jina la Saida Karoli.
Najua utakuwa unazikumbuka nyimbo mbalimbali zilizovuma toka kwake enzi hizo kama vile Maria Salome, Kaisiki, Ndombolo na Mimi Nakupenda.
Saida Karoli alizaliwa tarehe 4 Aprili, mwaka 1976 mkoani Kagera nchini Tanzania.
Hakubahatika kuendelea na masomo baada ya familia yake kushindwa kumsomesha.
Mwanzoni Saida Karoli alishindwa kujishughulisha na masuala ya muziki kwa sababu mila na tamaduni za ukoo wake hazikumruhusu kufanya hivyo.
Hata hivyo, mama yake ambae alikuwa na kipaji cha ngoma za kienyeji ndiye aliyempa moyo na hata kumfundisha masuala mbalimbali ya sanaa hiyo, hasa upigaji wa ngoma.
Uwezo wake mkubwa kwenye muziki uligunduliwa na kampuni ya FM Productions iliyokuwa ikisaka vipaji mkoani Kagera. Baada ya kuridhishwa na uwezo wa Saida Karoli, moja kwa moja ilimpeleka jijini Dar es Salaam ambapo ndani ya wiki tatu tu, aliweza kuachia vibao vikali vilivyotamba ndani na nje ya Tanzania kupitia albamu yake ya Maria Salome aliyoitoa mwaka 2001. Albamu hiyo ilitolewa chini ya mzalishaji maarufu wa kipindi hicho Mika Mwamba.
Albamu hiyo ilisheheni nyimbo kama vile Maria Salome au ‘Chambua Kama Karanga’, iliyokuwa na mahadhi ya Kihaya.
Ni kupitia albamu ya Maria Salome, Saida aliweza kuzuru nchi mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki na kujizolea maelfu ya mashabiki.
Pia alipata fursa ya kutumbuiza mbele ya Mfalme Kabaka wa Buganda. Mwaka uliofuata, Saida akaachia albamu nyingine yenye jina Mapenzi Kizunguzungu na kufanikiwa kuteka nyoyo za mashabiki wake kama ilivyokuwa katika nyimbo zake nyengine.
Baada ya kupotea kwa muda mrefu, Saida Karoli akaibuka tena mwaka 2017 na kibao cha Orugambo ambacho hakikuweza kufanya vizuri kama ilivyokuwa kwa Maria Salome na nyinginezo.
Wengi mtakumbuka wimbo wa Salome ulitolewa na Diamond na Rayvanny mwaka 2016 ambao ulikuwa na baadhi ya vionjo kutoka kwenye wimbo wa Saida Karoli uitwao Maria Salome.
Katika mahojiano yake na gazeti moja nchini Tanzania, Saida Karoli mwenyewe alinukuliwa akisema kuwa aliwahi kupata kiasi kisichozidi Dola za Kimarekani 380 baada ya wimbo wake kurudiwa.
Kwa sasa, Saida Karoli amehamishia maskani yake mkoani Mwanza nchini Tanzania ambako ndiko anapofanyia shughuli zake za muziki.