Vazi la khanga au leso lilivyofungamana na utamaduni wa waswahili
Vazi la khanga au leso lilivyofungamana na utamaduni wa waswahiliKhanga, au leso, ni kipande cha kitambaa chenye umbo la mstatili kilichotengenezwa kwa pamba na kupambwa kwa rangi tofauti, huku misemo na methali za Kiswahili zikitumika kutoa ujumbe.
Khanga ni vazi linalovaliwa sana Afrika Mashariki
27 Novemba 2024

Fathiya Bayusuf

TRT Afrika, Mombasa, Kenya

Khanga, au leso, ni kipande cha kitambaa chenye umbo la mstatili kilichotengenezwa kwa pamba na kupambwa kwa rangi tofauti, huku misemo na methali za Kiswahili zikitumika kutoa ujumbe.

Hii ni zaidi ya vazi tu; ni sanaa ya utamaduni na urembo, hasa kati ya wanawake wa Pwani ya Afrika Mashariki. Mara baada ya kuvaa nguo, mwanamke hujitwika leso kiunoni na kufunika kichwa, kujenga taswira ya utamaduni na heshima, nyumbani au kwenye sherehe mbalimbali.

Kwa wanawake, leso ni ishara ya heshima na mapenzi kutoka kwa waume zao. Kukusanya gora nyingi za leso kunamaanisha zaidi ya urembo; ni kielelezo cha matunzo na upendo katika ndoa.

"Leso ni kama pambo kwa mwanamke wa Kiswahili. Kila anapovaa leso, anapaa kwenye daraja la umuhimu na uzuri. Ni zaidi ya vazi la kihistoria lililovaliwa na wazee wetu, hasa ile aina ya Kisutu iliyokuwa maarufu kwenye matukio kama harusi au tamasha za kitamaduni," anasema Bi. Amira Msellem, mtafiti wa mila na tamaduni za Kiswahili, Mombasa.

Historia ya leso inaaminika kuanzia kwa Wareno katika Pwani ya Afrika Mashariki, hasa katika visiwa vya Unguja, Pemba, na Mombasa, karne ya 19. Kadri siku zilivyosonga, leso imepata umaarufu zaidi miongoni mwa Wapwani, na mitindo tofauti ya mapambo ikaanza kuibuka.

Mitindo ya awali ilikuwa ni madoadoa meupe na meusi, ikifanana na rangi za ndege wa mwituni anayeitwa kanga. Hapo ndipo jina "khanga" lilipoanza kuchipuka na kupendwa na watu.

"Khanga za mwanzo zilikuwa na madoa meupe na meusi tu, hazikuwa na maandishi yoyote. Lakini kadri wakati ulivyosonga, ziliboreshwa kwa mitindo mbalimbali," anasema Imran Abdul Haq, mbunifu wa leso katika duka la Abdullah, maarufu mjini Mombasa.

Kupita miaka, mitindo ya leso ilikua na kuongezewa ubunifu wa rangi, maua, na picha za kuvutia kama vile mimea na wanyama.

Mwanzoni mwa karne ya 21, maandishi ya Kiswahili, misemo, na methali ziliongezwa kwenye leso, ikidaiwa kuwa ni jitihada za mfanyabiashara maarufu, Kaderdina Haji Isaack, anayejulikana kama Abdulla, mwanzilishi wa biashara ya leso huko Mombasa. Imran Abdul Haq, mbunifu wa leso katika duka la Abdullah, anaelezea jinsi babu yake alivyofanikiwa kutofautisha bidhaa zake na kuunda nembo iitwayo "Mali ya Abdulla."

"Mzee Abdulla ndiye aliyeongeza maandishi ya Kiswahili kwenye mtindo wa leso na watu wa Mombasa wakapenda sana. Wanawake Waswahili wakaanza kutuma ujumbe kupitia maandishi kwenye khanga wanazovaa. Hivyo, tumefanikiwa kupanua biashara yake kutoka kwa khanga hadi kuwa duka kubwa linalouza bidhaa za Kiafrika kama vile kaniki, vikoi, vitenge, na vitu vyengine," anasema Imran Abdul Haq, mbunifu wa leso katika duka la Abdullah.

Awali, misemo kwenye leso, ingawa ilikuwa ya Kiswahili, ilikuwa inaandikwa kwa herufi za Kiarabu, na baadaye kwa herufi za Kirumi wakati matumizi ya khanga yalipopanuka kutoka kwa watu wa pwani na kuenea kote Afrika Mashariki. Lakini kuna tofauti kati ya leso za Kenya na Tanzania. Imran anasisitiza, "Leso zetu za Mombasa zinajulikana kwa upana, uzito, na ubora zaidi, ndiyo maana watu wengi wanazipenda."

Khanga sio tu vazi la kitamaduni, bali imekuwa sehemu ya utamaduni wa Waswahili na Waafrika kwa ujumla. Amira Msellem, mtafiti wa mila na tamaduni za Kiswahili mjini Mombasa, anaelezea jinsi khanga zimetumiwa kama njia ya mawasiliano. Maandishi yake hutumika kuonyesha upendo, kutoa shukrani, au hata kuelezea hisia za ugomvi.

"Wanawake wa Kiswahili wanapendelea kutumia leso kutoa ujumbe. Wanaponunua leso, huchagua maandishi kulingana na ujumbe wanaotaka kuwasilisha. Mathalani, leso za mwanamke aliyezaa zinaweza kuwa na ujumbe wa kongole kama vile 'Karibu mgeni' au 'Asante mama kwa malezi,'" anasema Bi. Amira Msellem, mtafiti wa mila na tamaduni za Kiswahili, Mombasa.

Kulingana na Amira, leso pia zilitumika kama rasilimali kwa wanawake, na wakati mwengine ziliashiria msichana kubaleghe na kuingia katika utu uzima.

"Leso zilitumika kama rasilimali kwa mwanamke, kwa sababu ilikuwa ni kawaida kwa mwanamke kumiliki gora nyingi za leso. Wanawake walikuwa wakitumia leso kama njia ya kujiondoa matatizo ya kifedha kwa kuziuza."

"Pia, leso ilikuwa ikitumika katika mawasiliano kati ya wanandoa, kwani mara nyingine wanawake walikuwa na shida kutamka maneno moja kwa moja kwa waume zao. Hivyo, mwanamke angekunja leso kwa miundo mbalimbali kuwasilisha ujumbe kwa mumewe. Kwa mfano, umbo la pembe tatu kitandani kunaweza kuwa njia ya kumjulisha mumewe kuwa yuko kwenye hedhi," anaeleza Bi. Amira, mtafiti wa mila na tamaduni za Kiswahili, Mombasa.

Baadhi ya leso hutumiwa katika sherehe za harusi, uja uzito, tohara, au hata mazishi. Wanawake pia hutumia leso kuwabebea watoto na hata wakati wa kuswalia.

"Leso ni muhimu sana kwa mwanamke, kwani ni vazi la stara na hutumiwa sana kwa kuswalia, kufanyia kazi nyumbani, au hata kubeba watoto mgongoni. Leso ni sehemu muhimu ya maisha ya Waswahili, kutoka kuzaliwa hadi kifo."

"Mwanamke anapojifungua, lazima avae leso za kuketia kwa muda wa arobaini. Pia, zilitumika katika malezi ya watoto na hata kama bembea la mtoto, ikifungwa chini ya kitanda. Leso pia hupewa kama zawadi kwa mwanamke aliyezaa au kwa bibi harusi," anasisitiza Bi. Amira Msellem.

Licha ya mabadiliko ya wakati, leso bado inaendelea kuwa kipande muhimu cha utambulisho wa Kiafrika. Leo hii, khanga zinashonwa kama nguo za kitamaduni, hutumika kama mapambo katika sherehe za harusi na matukio mengine ya kitamaduni. Pia, leso zimejumuishwa katika mitindo ya kimataifa ya mavazi. Hata hivyo, baadhi ya wanawake bado wanashikilia utamaduni wa kuvaa leso kama njia ya kuhifadhi asili yao.

"Bado ninatumia leso nyumbani kwa sababu ni sehemu ya utambulisho wa mwanamke wa Kiafrika. Ninazinunua zikizingatia ujumbe kwa ajili ya kuzitoa kama zawadi katika matukio mbalimbali kama vile sherehe za kuzaliwa, harusi, au hata kwa wazazi wangu.

Ningewasihi wanawake wenzangu wasiache kuvaa leso, kwani kwa kuvaa leso ni kujivunia na kuheshimu asili yetu," anahitimisha Kavira Neema, raia wa Congo anayeishi Mombasa.

Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us