Rais wa Marekani Donald Trump, amelazimika kukatisha mazungumzo yake na Rais wa Volodymyr Zelenskyy baada ya kutokea majibizano makali ndani ya Ikulu ya Marekani, siku ya Februari 28.
"Leo tulikuwa na kikao muhimu ambacho kilishindwa kufikia muafaka.
Naona Rais Zelenskyy hataki kuona amani ikipatikana kwa kuwa Marekani imehusishwa, anadhani uwepo wetu unampa faida kwenye mazungumzo," alisema Trump katika taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii.
"Sitaki faida, nataka AMANI. Ameidharau ofisi yangu japo anakaribishwa wakati mwingine atakapokuwa tayari," aliongeza.
Kauli hizo zinakuja baada ya kutokea majibizano makali kati ya Trump, Zelenskyy na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, ambaye alimshutumu kiongozi huyo wa Ukraine kwa kukosa fadhila kwa watu wa Marekani katika kumaliza vita.
Zelenskyy alitarajiwa kupata mlo wa mchana na Rais Trump huku viongozi hao wakitia saini makubaliano ya mradi wa madini.
Badala yake, Zelenskyy alipanda gari lake na kuondoka zake.
Trump alimuomba Zelenskyy kuondoka Ikulu baada ya majibizano hayo, kulingana na chombo cha habari cha Fox.
Inaripotwa kuwa maofisa wa Ikulu walifurahia majibizano hayo.
"Litakuwa jambo kubwa kwenye televisheni,"alisema Trump baada ya kikao hicho kuvunjika.
Muda mfupi baadaye, timu ya mawasiliano ya Ikulu ya Marekani ilirusha video hizo kwenye mitandao ya kijamii.
"Siku zote, Rais Trump na Makamu wa Rais Vance watakuwa upande wa Marekani na wale watakaoheshimu misimamo yetu ulimwenguni. Hata siku moja hatutokubali kuchukuliwa kirahisi," alisema Margo Martin, mshauri maalumu wa Rais.
Dakika 10 za mwisho za mazungumzo hayo ya dakika 45 iligeuka kuwa majibizano makubwa.
Ilianza kwa Vance kumwambia Zelenskyy, "Mheshimiwa Rais, kwa heshima na taadhima, nadhani unatukosea heshima ndani ya Ikulu yetu na mbele ya vyombo vya habari."
Zelensky alijaribu kumkatisha Trump, kabla ya Rais wa Marekani kumwambia kuwa "Anayaweka maisha ya watu rehani."
"Unahatarisha kutokea kwa Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, unaikosema heshima nchi hii, nchi iliyokuunga mkono kuliko yeyote yule," alisema Trump.