Kuanguka kwa utawala wa Bashar al Assad kumetoa fursa kwa mamilioni ya wakimbizi na familia zao. Haya ndiyo matamshi ya Inas al Hachem kuhusu baba yake, ambaye aliondoka mji wa Aleppo lakini alikuwa na matumaini kuwa siku moja atarejea.
Bado nakumbuka safari yangu ya kwanza ya Aleppo, Syria, tarehe 28 Juni, 2001. Nilikuwa na umri wa karibu miaka saba. Shule zilikuwa zimefungwa nchini Uhispania, na kama ilivyo kwa jamii nyingi za watu wa Syria zinazoishi nje ya nchi, baba yangu,Fathallah, alikuwa anaweka akiba kila mwaka kwa ajili ya safari hii.
Gharama ya safari hii ilikuwa juu sana, hasa kwa familia kubwa kama ya kwetu. Lakini muda wote alikuwa akitueleza kuhusu Syria: kuhusu mji wa Aleppo, na hasa eneo la Al-Bab, Pamoja na watu wake, kuwepo kwa makabila mbali mbali na dini tofauti, historia yake. Na alijitahidi kuhakikisha kuwa tunaipenda na kuienzi ardhi yetu.
Alisema ni muhimu kupenda mji wa Madrid, lakini tusisahau asili yetu tulikotoka. Alikuwa na ndoto kuwa siku moja atarejea katika taifa la Syria litakalokuwa huru. Alitamani kuanzisha miradi ya hospitali, shule, miskiti na vituo vya kusaidia watu.
Lakini ilikuwa ni ndoto isiyowezekana, na alifahamu hilo. Syria imepitia kipindi kigumu sana chini ya utawala wa chama cha Baath, na baba yangu, kama ilivyo kwa wengine wengi, alilazimika kuondoka nchini 1969. Hakupendelea kufanya hivyo, lakini hakuwa na njia mbadala.
Kwa msaada wa familia yake na jitihada zake mwenyewe, alifanikiwa kukamilisha masomo yake ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Complutense cha Madrid, wakati huo huo akifanya kazi kujisaidia kimaisha. Muda wote alikuwa anawaza kuhusu Syria. Mara nyingi katika mazungumzo yake alizungumzia suala la ukombozi kwa watu wake.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe
Turejee katika safari yangu ya kwanza nchini Syria. Nakumbuka namna ilivyoacha athari kubwa kwangu. Kila kitu kilikuwa kinapendeza /kinavutia/kinashangaza, lakini kilichonishtua zaidi ni picha za dikteta zilizokuwepo kila sehemu.
Kwa sikufahamu, nikauliza kwa nini picha zake ziko kila mahali. "Usizungumze kwa sauti ya juu," mama yangu aliniambia na kaka yangu pia, ambaye yeye alikuwa amejifunza kutokana na safari zake za awali nchini humo. Ilikuwa ni kama hairuhusiwi kumtaja Assad, kama humtaji kwa kumsifu.
Wakati wa harakati za mapinduzi zilipoanza mwaka 2011, ilionekana kama ndoto isiyowezekana. Tuliishi tukiwa na matumaini kuwa siku moja mambo yatabadilika na kuwa mazuri. Tulifwatilia taarifa za habari kila siku – muda wote tukitizama Al Jazeera.
‘’Hatukudhani kuwa mapambano haya yangechukua muda wa miaka 14 na kwamba baba yangu hatokuwepo hai kushuhudia. Alifariki dunia miaka mitatu iliyopita.
Kwanza, mawasiliano na familia yetu ilikuwa ni kuwapa matumaini na kufahamu hali ilivyo, lakini mambo yakageuka na kuwa mikosi: mabomu, kukamatwa, kupotezwa. Tulipoteza watu wengi sana.
Mjomba wangu Mahmoud, alikuwa daktari wa mifugo na baba wa watoto sita, aliuawa kwa bomu wakati akiwa katika maandamano mjini Aleppo. Binamu zangu wawili, Firas na Hasan, walipotea, na hata hatukupata miili yao tuizike. Mtoto wa kiume wa binamu yangu Amani, Ali Rakan, akiwa na umri wa miaka 14 tu, aliuawa kikatili na huo utawala wakishirikiana na vikosi vya Urusi. Na mjomba wangu mwingine pia alikamatwa.
Kwa muda mrefu, watu walikata tamaa zaidi ya kuwa na matumaini. Lakini muda wote baba yangu alikuwa na matumaini. Kila hatua ambayo wapinzani walipiga, kwake ilikuwa, "hatua muafaka."
Alikuwa akisema ushindi uko karibu. Hatukudhania kuwa mapambano yangeendelea kwa mud awa miaka 14 na kwamba baba yangu hatokuwepo kushuhudia ushindi huu, kwa kuwa alifariki dunia miaka mitatu iliyopita.
Mwisho wa Assad
Kisha siku ya Jumapili, kila kitu kikabadilika. Usiku wa tarehe 8 Disemba hautosahauliwa. Wakati taarifa za wapinzani kufika mji mkuu wa Damascus, zilipotufikia saa kumi na moja na nusu alfajiri, baada ya kulala kwa saa mbili pekee. Tuliifahamu kuwa hii inamaanisha mwisho wa Assad.
Ungetuona mimi na kaka yangu hapa mjini Istanbul tunaangalia televisheni kufwatilia taarifa hizo. Taarifa zaidi katika mitandao ya Twitter na Instagram. Familia kuwasiliana na sisi kwa njia ya video — baadhi yao wakiwa Madrid, wengine Qatar, Norway, Syria, Ujerumani … kote duniani. Tulisherehekea kila hatua iliyopigwa na wapinzani.
Saa tisa unusu usiku, nilikuwa nimelala usingizi wa mang’amung’amu, mara kaka yangu akaniamsha saa mbili baadaye, akipiga kelele kwa furaha: "Bashar amepinduliwa ! Bashar amepinduliwa!" Ilikuwa ni furaha kubwa ambayo siwezi kuielezea. Vicheko, machozi, pambaja. Hatukuweza kulala tena.
Tulienda katika mtaa wa Fatih, jijini Istanbul, sehemu ambayo wakimbizi wengi kutoka Syria wanaishi. Watu walikuwa wanatoa vyakula vitamu, hasa halawet el jibn, chakula kitamu maarufu ambacho huliwa wakati wa sherehe maalumu.
Wengine walikuwa wanaimba "Sisi tuko pamoja,tuko Pamoja … watu wa Syria tuko pamoja" huku wakisherehekea. Licha ya kutojuwana, siku hiyo tulikuwa kama familia moja. Tulipongezana. Baada ya maumivu ya muda mrefu, tuliungana kusherehekea ushindi wetu sote, tukiwa na matumaini.
Hatimaye, raia wa Syria wanastahili kuwa na furaha tena. Hatimaye sisi siyo "wakimbizi" tena, tumekuwa watu wenye ardhi yao, iliyo na jina na tuna ndoto.
Tayari kwa mustakabali
Syria, au kama tunavyopenda kuiita, Sham, nchi ya asumini, itakumbukwa kwa uzuri wake,historia yake, ustaarabu wake wa tangu enzi, utamaduni wake wa thamani, na siyo vita vyake.
Najuwa mambo hayatokuwa rahisi. Kujenga nchi baada ya vita si jambo rahisi. Lakini angalau kwa mara ya kwanza, tumepata jambo la kufurahia na matumaini kwa mustakabali wetu.
Nadhani kwa wote wale tuliowapoteza, wale waliojitolea kwa hili, kutoka kwa Hamza al-Khatib, shahidi wa kwanza wa mapinduzi , aliteswa na kuuawa huko Daraa kwa kudiriki kuandika neno "uhuru’’ kwenye ukuta, hadi Abdul Baset al-Sarout, aliyekuwa ishara ya mapambano.
Golikipa wa zamani wat imu ya taifa ya Syria,sauti yake iliwahamasisha watu wengi Homs, jambo la kishujaa ambalo lilimsababishia yeye kupoteza maisha yake.
Nikifkiria kuhusu baba yangu natabasamu, kwa sababu najuwa na yeye anatabasamu pia. Namshkuru Mungu.
Na naam, tayari tunapanga safari nyingine. Kwa sababu sasa, hatimaye, tunaweza kwenda Syria na Aleppo tena. Naam, kwa faida yetu sisi, lakini hasa kwa ajili yake.
Awali makala haya yalichapishwa na TRT Espanol.
CHANZO: TRT World