Karibu uandamane nami hadi kwenye visiwa vya karafuu, yaani Zanzibar ambako ndio chimbuko la muziki wa Taarab; na leo hii tukiwa tunamuangazia Malkia wa Muziki huo, Khadija Omar Kopa.
Akiwa amezaliwa mwaka 1963 katika mtaa wa Makadara visiwani Zanzibar, alipenda sana kughani kaswida pamoja na kuimba kwaya shuleni.
Mnamo miaka ya tisini, ndoto zake zilianza kutimia na kuanza kuimba taarabu asilia, baada ya kujiunga na kikundi kikongwe cha taarabu huko Zanzibar cha Culture Musical Club.Kipaji chake kilizidi kung’aa alipojiunga na Muungano Cultural Troupe na baadaye, Tanzania One Theatre (TOT), kilichokuwa kinaongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wafuatiliaji wa muziki huu watakumbuka vizuri kwenye miaka ya mwishoni ya 90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, upinzani wa makundi mawili ya Muungano na TOT; kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na uwepo wa Khadija Kopa kwa upande wa TOT, na Nasma Khamisi ‘Kidogo,’ kwa upande wa Muungano.
Ushindani wa Khadija na Nasma ulipamba moto baada ya Kopa kuchukuliwa na Bendi ya TOT kutoka katika Bendi ya Muungano na zilitungwa nyimbo nyingi za kupigana vijembe kama vile "Mtu mzima hovyo," ambayo Nasma alimtungia Khadija, kabla ya Khadija kujibu na kitu “Y2k Manjonjo," mwanzoni kabisa ya mwaka 2000.
Kimsingi mtifuano kati ya Khadija na Nasma ulifanya vikundi vya TOT na Muungano viwe moto sana nyakati zile, kwa maelezo ya Khadija Kopa, alishawahi Kusema Nasma Khamisi, alikuwa ni hasimu wake kwenye muziki tu, lakini nje ya muziki walikuwa ni marafiki, na walishirikiana mambo mengi mbalimbali.“TX Mpenzi”, Gwiji, , “Top in Town”, “Unaringa Umepima”, “Mambo Iko Huku”, “Tutabanana Hapahapa” na nyingine nyingi tu zilizompa Umalkia wa Mipasho ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Mbali na kushiriki kutunga nyimbo za Taarab kwa ajili ya kikundi cha TOT, Khadija Kopa pia alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alishirikiana na Kapteni Komba kutunga nyimbo za hamasa za chama hicho pamoja kuendeleza vipaji vya utunzi, uimbaji, uchezaji ala na uigizaji.
Akiwa TOT Taarab, Khadija Kopa aliingia kwenye mahusiano na mtunzi na mwimbaji mwingine wa kikundi hicho aitwaye Othman Soud, na wakabahatika kupata mtoto, ambaye leo anajulikana kama Zuhura Othman Soud, maarufu kama Zuchu.Mbali na Zuchu, Malkia huyo wa mipasho pia aliwahi kuwa na mtoto mwingine aitwaye Omary Kopa ambaye alifanya vizuri sana katika Taarab kupitia nyimbo zake kama vile ‘Imetulia Hiyo’ na ‘Nipepe’, kabla ya kufariki mwaka 2008.
Katika muziki huo Khadija Kopa ameshapata tuzo nyingi sana zikiwemo zile maarufu za Kilimanjaro Tanzania Music Awards, na tuzo za Afrimma akiwa ni msanii pekee wa taarab aliyeshiriki tuzo hizo katika kipengele cha mwanamke bora Afrika Mashariki na Kati.
Kwa sasa, Khadija Kopa ni kama amepumzika shughuli za kuimba, japo amekuwa akishirikishwa sana na wasanii wa muziki wa Bongo Fleva, akiwa tayari amefanya kazi na Chid Benzi, Diamond Platnumz, Aslay na binti yake mwenyewe, Zuchu.