Ulimwengu
4 dk kusoma
Wanafunzi wa Syria masomoni Uturuki:ushirikiano wa kidiplomasia
Wanafunzi wa Syria walio katika vyuo vikuu nchini Uturuki wameonesha ishara ya namna diplomasia inavyoimarishwa na kutoa mtazamo wa ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Wanafunzi wa Syria masomoni Uturuki:ushirikiano wa kidiplomasia
Uturuki imejizatiti kama sehemu muhimu ya masomo ya juu dunia ikitajwa hivi karibuni kama nchi ya saba maarufu kwa wanafunzi kutoka nje.
27 Februari 2025

Na Faruk Tasci

Katika madarasa yaliyo wanafunzi kwenye vyuo vikuu vya Uturuki, kuna ushirikiano wa kidiplomasia unaoimarishwa. Wanafunzi wa kimataifa wameongezeka mara sita zaidi katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, kwa sehemu kubwa wakiwa wanafunzi kutoka Syria.

Miongoni mwa wanafunzi 336,000 wa kimataifa nchini Uturuki, zaidi ya 60,000 wanatoka Syria, kuwafanya kuwa kundi kubwa la wanafunzi wa kigeni nchini. Hili ni ongezeko la mara thelathini zaidi tangu 2013, wanafunzi wa Syria wakiwa humusi ya wanafunzi wa kimataifa.

Wanafunzi hawa ni zaidi ya uwekezaji katika elimu — ni kiunganishi muhimu kati ya Uturuki na na Syria mpya baada ya vita, wakionesha ushirikiano wa mataifa hayo mawili katika maeneo zaidi ya darasani.

Kuteuliwa kwa waziri mpya wa mambo ya nje wa Syria, Asaad Hassan al Shaibani— mhitimu wa chuo kikuu cha Istanbul Sabahattin Zaim — anaonesha hili.

Shaibani, ambaye bado anafanya shahada ya uzamivu kwenye chuo hicho, alifanya shahada yake ya uzamili kuhusu sera ya mambo ya nje ya Uturuki kuhusu Syria, ikiwa ni ishara ya kudhihirisha ushirikiano katika taaluma na kubadilishana mawazo ya kisiasa.

Hayuko peke yake: Gavana mpya wa mji wa Aleppo aliyeteuliwa, Azzam al-Gharib, pia amesoma elimu ya dini ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Bingol mashariki mwa Uturuki.

Wahitimu hawa, ambao wanachangia pakubwa katika mwelekeo mpya wa siasa za Syria, wanadhihirisha kile msomi wa Marekani Norman Kiell amekitaja 1951 kuwa “mabalozi wasiyo rasmi”.

Na huku wanafunzi zaidi wa Syria wakirejea nyumbani, ni wangapi watakuwa katika nafasi zenye ushawishi, watakaokuwa siyo tu na elimu lakini pia ufahamu wa mtazamo wa kimkakati wa Uturuki.

Idadi nyingine kubwa ya wanafunzi inatoka Azerbaijan, Iran, Turkmenistan, na Iraq, kuonesha ushirikiano wa Uturuki katika suala la elimu kwenye kanda nzima.

Kutoka kuwa wanafunzi hadi wanadiplomasia, wafanyabiashara, na wanazuoni

Mbali na siasa, hawa wanafunzi wanaimarisha ushirikiano katika nyanja za uchumi na utamaduni kati ya Syria na Uturuki.

Kulingana na shirika la mipango la Istanbul (IPA), wanafunzi wa kimataifa wanachangia tarkiban dola bilioni $2.9 kwa uchumi wa Uturuki kila mwaka, huku wanafunzi wa Syria wakichangia karibu dola milioni $522.

Mwaka uliopita, akiwa katika hafla ya Chuo Kikuu cha Marmara Istanbul, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, alisisitiza kuhusu ushawishi unaongezeka wa wanafunzi wa kimataifa nchini Uturuki, wakiwa wanachangia uchumi wa nchi na kiunganishi kwa ulimwengu. Alibainisha kuwa asilimia 95 huwa wanajilipia ada ya masomo, ukweli ambao unadhihirisha kuibuka kwa Uturuki kama kitovu cha elimu duniani.

Kuongezeka kwa idadi ya vyuo vikuu kutoka 76 mwaka 2002 hadi 208 na kutoa fursa za ufadhili wa masomo kupitia YTB kumefanya Uturuki kuwa sehemu ya saba maarufu duniani kupata masomo ya juu baada ya Marekani, Canada, Uingereza, Australia, Ufaransa na Ujerumani.

Kuwepo kwa wanafunzi wa kimataifa na wahitimu tayari kunaimarisha ushirikiano thabiti wa biashara, huku wahitimu wanaofahamu soko la Uturuki na taratibu za biashara wakiendeleza ushirikiano huo wa biashara wanaporejea kwao.

Kwa sehemu kubwa, wanajiweka katika nafasi ya kuwa “mabalozi wa biashara” wa Uturuki katika kipindi cha ujenzi mpya wa Syria.

Ulimwengu wa elimu pia unabadilika.

Kuwepo kwa wanafunzi zaidi ya 60,000 wa Syria kumeimarisha masomo ya elimu ya juu ya Uturuki, na kufanya mazingira ya masomo kuwa ya kimataifa.

Huku wahitimu hawa wakianza kufanya kazi katika taasisi za Syria, bila shaka kutakuwa na ushirikiano mkubwa katika masuala ya masomo, utafiti, na mambo ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili.

Ili kufanikisha hili moja kwa ukubwa wake, Uturuki inaweza kuanzisha “mkakati wa wanafunzi na wahitimu wa Syria”.

Kwa kuangalia uhalisia wa mambo, Uturuki inatakiwa kuchukua muelekeo wa kimkakati — ambao utachagiza mtandao wa wahitimu wa Syria, kama ambavyo Marekani na Uingereza imekuwa ikifanya kwa miongo kadhaa.

Kuna wahitimu wa vyuo vikuu vya Marekani wasiopungua 54 na ambao ni viongozi katika mataifa yao. Hivyo hivyo kwa Uingereza, ambapo wana kiongozi mmoja kutoka nchi 53.

Uturuki ni mfano wa kuigwa.

Ili kuimarisha ushirikiano na wanafunzi wa kimataifa ambao wanachangia katika sekta zaidi ya moja, Uturuki inatakiwa kujenga mitandao itakayoimairisha uhusiano wa wahitimu hawa. Hii itahakikisha mawasiliano ya moja kwa moja na ushirikiano, pasipo na kuingiliwa na makundi mengine yoyote.

Kwa kuwekeza kwa hawa wanafunzi, Uturuki siyo tu inaelimisha kizazi— inajenga msingi wa kudumu wa ushirikiano wa kikanda.

Uturuki inajiweka katika nafasi yake kama eneo muhimu la kupata elimu duniani, wanafunzi hawa hawaimarishi tu uchumi lakini pia jukumu la nchi katika masuala ya diplomasia ya utamaduni.

Mwandishi, Profesa Faruk Tasci ni Mkurugenzi wa Kituo cha wanafunzi wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Istanbul.

Angalizo: Maoni haya ya mwandishi hayaakisi maoni, msimamo au sera ya uhariri ya TRT Afrika.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us