Maisha
6 min read
Hati ya kukamatwa kwa jenerali wa Myanmar inafufua vita vya haki vya Rohingya
Kiongozi wa kijeshi Min Aung Hlaing anashtakiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa mauaji ya kimbari ya Rohingya 2017. Hatua hiyo inatoa nafasi muhimu kuelekea uwajibikaji, ingawa haki bado haijafikiwa.
Hati ya kukamatwa kwa jenerali wa Myanmar inafufua vita vya haki vya Rohingya
Kamanda mkuu wa jeshi la Myanmar, Jenerali Mwandamizi Min Aung Hlaing, akihudhuria mazoezi ya kijeshi katika eneo la delta ya Ayeyarwady nchini Myanmar, Februari 3, 2018. / Picha: Reuters
27 Februari 2025

Na Hannan Hussein

Katika hali ya kushangaza wiki iliyopita, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliomba hati ya kukamatwa kwa Min Aung Hlaing, kiongozi wa kijeshi wa Myanmar na mhusika mkuu wa mauaji ya kimbari ya mwaka 2017 dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Miaka saba baada ya kampeni ya kufurusha Warohingya kwa misingi ya ukabila kuanza, hatua hiyo inaweza kutoa faraja baridi kwa jamii iliyofungiwa nje ya nchi yao.

Zaidi ya Warohingya milioni moja walilazimika kuikimbia Myanmar mwaka 2017 baada ya jeshi kuteketeza vijiji na kuendesha kampeni ya mauaji ya halaiki, ubakaji na kuwafukuza maelfu ya wanajamii.

Min Aung Hlaing, ambaye anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, anatuhumiwa kuendeleza mauaji ya kikabila na kuyaficha kisirisiri.

Makumi ya maelfu waliuawa wakati walionusurika walitawanyika katika kambi za wakimbizi katika nchi jirani ya Bangladesh. Wengi wamesalia katika kambi zilizokua na msongamano wa watu, vituo visivyo na ufadhili wa kutosha, wakiendelea kukabiliana na ukiukwaji wa haki unaoendelea.

Sasa wakati jeshi la jenerali huyo likifanya ukatili zaidi dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine magharibi, kibali cha ICC ni muhimu katika kupinga kutokujali kwa jeshi hilo.

Junta inaweza kusema kuwa si nchi mwanachama wa ICC, na haiwajibishwi na matendo yake. Lakini hiyo haibadilishi ukweli kwamba ICC inaweza kuchunguza uhalifu wa kijeshi wa kuvuka mpaka dhidi ya Warohingya katika nchi jirani ya Bangladesh, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza nchini. Kwa hivyo, hati hiyo inahakikisha kwamba harakati za haki zinabaki hai.

Ukatili wa Kutisha

Kama mhusika mkuu wa mauaji ya halaiki ya 2017, kukamatwa kwa Min Aung Hlaing kunaweza kuwa hatua muhimu katika kutafuta haki kwa watu wa Rohingya. Kwa miaka mingi, jeshi la Myanmar limefanya kila juhudi kuweka mauaji ya kimbari ya Warohingya kwenye msukosuko.

Hati ya kukamatwa ni hatua muhimu kuelekea kutoboa ngao hii ya kutokujali. Ilikuwa chini ya uongozi wa jenerali ambapo jeshi liliendeleza uhalifu wa kutisha, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia ulioenea na kuwafukuza Warohingya kutoka nchi yao.

Kutokuwepo kwa uwajibikaji wa kimataifa kumeruhusu uhalifu kama huo kuendelea bila kudhibitiwa, na kusababisha kovu kubwa kwa vizazi vya Rohingya. Tangu 2017, matokeo ya ukatili huu yamekuwa makubwa.

Tazama Bangladesh, ambapo idadi kubwa ya Warohingya walihamishwa kwa nguvu. Zaidi ya milioni moja wamesalia kufungwa katika kambi za wakimbizi zilizojaa kupita kiasi. Kwa waliokimbia makazi yao, ahadi ya usalama inabaki kuwa ya uwongo, kwani wanaendelea kung'ang'ania kutambuliwa na haki ya kurudi nyumbani.

Ukweli huu wa kutisha ni matokeo ya moja kwa moja ya kampeni ya Min Aung Hlaing ya kuwafurusha kwa wingi. Na kwa hivyo, kukamatwa kwake kusingeanza tu kushughulikia miaka ya dhulma iliyovumiliwa na Warohingya, lakini pia kutuma ujumbe wenye nguvu kwa maafisa wengine wa kijeshi waliohusika katika mauaji ya halaiki kwamba hakuna mtu asiyeweza kufikiwa na sheria.

Hebu tuwe wazi. Kutochukuliwa hatua duniani kumewapa ujasiri jeshi la Myanmar katika kuendeleza ukatili wake. Min Aung Hlaing kwa sasa anaripotiwa kusimamia ongezeko la mauaji makubwa ya Warohingya, na kuendeleza mfumo wa ubaguzi wa rangi unaowaweka maelfu ya Warohingya kwenye maisha ya kunyimwa haki kwa njia iliyoratibiwa.

Kutafuta uwajibikaji

Kushindwa kwa vyombo vya kimataifa, likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutoa shinikizo la maana kwa serikali ya kijeshi kumewaacha viongozi wa Rohingya wakiwa wamekata tamaa na madai yao ya haki kutotekelezwa.

Hati ya kukamatwa kwa ICC, hata hivyo, inatoa mwanga wa uwajibikaji, ikitoa fursa muhimu ya kuvuruga hali ya kutokujali ya junta iliyoenea. Miaka ya stakabadhi za ushahidi uliorekodiwa unapinga moja kwa moja majaribio ya Min Aung Hlaing ya kuzuia mauaji ya 2017 yasijulikane.

Uongozi wake haukuacha juhudi zozote katika kuwachafua watu wachache wa Rohingya, na kujenga mazingira ambapo Mabudha wenye msimamo mkali waliratibu mauaji ya halaiki pamoja na wanajeshi.

Uzito wa ukatili unaoongozwa na serikali ulipuuzwa sana kwa miaka mingi, na kwa kumaanisha, mateso ya Warohingya pia yalipuuzwa sana.

Mashirika ya haki za binadamu yanaweza kufarijiwa na ukweli kwamba kibali hiki ni hatua muhimu kuelekea kutekeleza shinikizo kwa serikali ya kijeshi.

Kibali cha kushikwa kwa Min Aung Hlaing kinaweza kuwa alama ya uidhinishaji wa hadhi ya juu zaidi dhidi ya mjumbe wa serikali ya kijeshi ya Myanmar, na kuongeza matarajio ya vibali zaidi dhidi ya wasaidizi walio chini yake waliohusika katika mauaji ya halaiki.

Inatosha

Kwa kweli, tangazo la ICC lina maana ndogo kwa wale wanaoteseka nchini Myanmar na Bangladesh.

Lakini mwendesha mashtaka mkuu Karim Khan amesisitiza udharura wa kuweka kikomo kwenye mauaji ya kimbari ya jeshi la Myanmar huko Rakhine, akifichua kwamba vibali vya ziada viko njiani. Pia amesisitiza kwamba Warohingya na vita vyao vya kupigania haki "havijasahaulika."

Sehemu ya mapambano hayo itamaanisha kukomesha aina zote za mateso na ukatili dhidi ya Warohingya wapatao 630,000 wanaodhulumiwa nchini Myanmar.

Ushahidi kutoka kwa Human Rights Watch (HRW) umeonyesha kuwa jeshi la Myanmar limejitolea kufanya mashambulizi ya kiholela dhidi ya wanajamii, na limeajiri wanaume wa Rohingya kinyume cha sheria kutumikia kampeni kubwa ya vita vya junta katika jimbo lao la asili.

Ahadi za haki na uwajibikaji zimesalia kuwa kilio cha mbali wakati Min Aung Hlaing atakapoweza kudumisha hali ya mateso ambayo yanaendelea zaidi hata baada ya 2017 na kuendelea hadi leo.

Hili ni muhimu kwa sababu ICC inachunguza uhalifu uliofanywa katika miezi ya mwisho ya 2017. Lakini hata kama tishio la kibali cha kukamatwa likizidi kuwa kubwa, ni kidogo sana kinachozuia jeshi kuendeleza mauaji ya kimbari hadi mwaka ujao.

Mashirika mengi ya kutetea haki za Warohingya yanasema kwamba vibali vya ICC lazima vifanya kazi yake ili kuchukua hatua halisi. Kusubiri kumekuwa kwa muda mrefu sana: wanaharakati, mashahidi na walionusurika wametumia miaka mingi kushinikiza uchunguzi uliofanywa uchukuliwe hatia.

Mchakato unabaki kuwa wa polepole na umejaa changamoto. ICC inaweza kuchukua hadi siku 100 kukamilisha hati dhidi ya Min Aung Hlaing, na mashtaka halisi yanaweza kuchukua miaka. Zaidi ya hiyo ni kwamba Min Aung Hlaing husafiri ng'ambo mara chache sana. Uwepo wake katika nchi yoyote kati ya nchi 124 wanachama wa ICC ni jambo muhimu la kuzingatia ili kukamatwa.

Hata hivyo, kibali ni zaidi ya hatua ya kiutaratibu. Kwa utawala wa kijeshi ambao kwa utaratibu umepanga mauaji, ubakaji na kufukuzwa kwa lazima kwa Warohingya, kibali cha ICC ni jaribio la maana la uwajibikaji wa muda mrefu.

Manusura wa mauaji ya halaiki kwa muda mrefu wamekuwa wakibishana juu ya hatua ya kuanzia ambayo inaweka ngao ya jeshi ya kutokujali. Hati ni hatua hiyo ya kuanzia - ishara kwa ulimwengu kwamba uhalifu dhidi ya Rohingya hautapuuzwa na kwamba haki, ingawa imecheleweshwa, bado ni lengo linaloweza kufikiwa.

Mwandishi, Hannan Hussain ni Mtaalam Mwandamizi katika Initiate Futures, mwandishi kutoka Islamabad. Alisomea Usalama wa Kimataifa kupitia Fulbright katika Chuo Kikuu cha Maryland, na amekua mshauri na Taasisi ya New Lines ya Mikakati na Sera huko Washington. Makala ya Hussain imechapishwa na Carnegie Endowment for International Peace, Georgetown Journal of International Affairs, na Express Tribune (mshirika wa International New York Times).

Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.

Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us