Rais wa Kenya William Ruto ametoa ujumbe maalum kuwatakia heri Waislamu kote nchini wanapojiandaa kuanza kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.
“ Tunakumbushwa thamani na umuhimu wa kipindi hiki takatifu. Ramadhan sio tu mwezi wa kujizuia na starehe bali ni wakati wa ibada, sadaka, ukarimu na tafakari ya kina,” Rais Ruto ameongezea.
Amewakumbusha Waislamu kwamba huu ulikuwa wakati muhimu wa kutafakari kiimani, nidhamu binafsi, na kujitolea kufanya hisani zaidi.
“Ni fursa adhimu ya kila mmoja kujitakasa nafsi, kuimarisha imani na kujitolea katika matendo ya haki.” amesema.
“ Mnapoanza safari hii ya kiroho nawahimiza muombee nchi yetu na raia wake. Muwafikirie na kuwasaidia wale wasiojiweza. Na mdumishe maadili ya huruma mshikamano wa kujitolea kwa ajili ya wenzenu,” Rais Ruto amesema akiwatakia Waislamu Ramadhan Mubarak.