Burundi ni nchi ya Afrika Mashariki inayopakana na Rwanda kwa upande moja, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na Tanzania.Katika nchi hii yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 13, ngoma si ngoma tu, ngoma inachukuliwa kama kitu kitakatifu na ishara ya heshima.
Utamaduni wa upigaji ngoma unaojulikana kienyeji kama "ingoma" ulianza karne ya 17, na uliheshimu utawala wa familia ya kifalme wakati huo.
Ngoma hiyo, ilipigwa baada ya mfalme kuchukua kiti cha enzi, na ilionekana kuwa chanzo cha nguvu zake. Ngoma zilichezwa kuashiria mwanzo na mwisho wa shughuli za kifalme za kila siku, sherehe tofauti kama karamu ya mbegu mfalme alipobariki watu wake na kufungua msimu wa kilimo.
Tambiko jengine ni pamoja na kuashiria kifo cha mfalme na kuzinduliwa kwa ufalme mpya. Ngoma zilipigwa kuonyesha kwamba maisha mapya yalianzia kwenye jumba la kifalme. Miaka mingi baadaye, ngoma za Burundi bado zina umuhimu mkubwa.
Wanaume hurithisha watoto wao wa kiume ujuzi wa kupiga ngoma. Ingawa ngoma nyingi zimetoweka kwa miaka mingi lakini mbili zinazojulikana kama Ruciteme na Murimirwa zimehifadhiwa katika kibanda cha jadi cha majani huko Gishora.
Zinaaminika kuwa na zaidi ya miaka 118. Gishora iko juu ya kilima, takriban kilomita 7 kutoka mji wa Gitega. Eneo hili linatunzwa na jamii ya wapiga ngoma wanaoitwa Abatimbo. Hapa vijana na wazee wanajifunza ustadi tofauti wa kucheza na pia kucheza densi kulingana na midundo ya ngoma.
Hii inahusisha kutengeza maumbo tofauti ya mwili na kuruka juu. Kwa muda mrefu, ngoma hizi zingeweza tu kuchongwa kutoka vigogo vikubwa vya "umuvugaangoma", au "mti unaofanya ngoma izungumze."
Kutokana na ubora wake, tangu mwaka wa 2014, ngoma hii ya Burundi inatambulika sasa kimataifa. Hii ni baada ya Shirika la Umoja Mataifa la Utamaduni UNESCO kuiorodhesha kama urithi wa utamaduni.
Na ili kuupa nguvu utamaduni huu, Serikali ya Burundi imepiga marufuku ngoma hizi kupigwa bila idhini ili kulinda mila zinazoendana na ngoma za taifa hili.
Moja wapo ni mwiko kwa mwanamke yoyote kuzipiga kama ilivyokuwa wakati wa ufalme ikidaiwa kwamba ngoma kwenye muundo wake ina "viungo na maumbile" ya mwanamke.
Aidha Serikali ya Burundi imepiga marufuku upigaji wa ngoma katika mikutano isiyokuwa rasmi ikiwemo sherehe za kitamaduni na harusi katika jaribio la kuhifadhi mila hiyo ya zamani ambayo sasa inajulikana kimataifa.
Na tangu mwaka wa 2017 serikali iliazimia pia uwepo wa ada za kulipia upigaji wa ngoma kwenye sherehe mbalimbali ikiwa ni franka za Burundi laki tano sawa na dola 165.
Kwa hivyo sasa, tunapowaona wale wanaume ambao wanabebea ngoma kubwa kubwa wakiwa wamevalia sare za bendera ya Burundi, tuwape heshima kwani wanayocheza si ngoma ya kututumbuiza tu, bali wanawakilisha ishara kubwa ya nchi yao .