Afrika
2 dk kusoma
Rwanda yaambia nchi za Ulaya zisichanganye siasa na masuala ya usalama.
Februari 24, bunge la mataifa ya Ulaya lilijadili uwezekano wa kuiwekea Rwanda vikwazo. Wabunge walifikia makubaliano ya awali tu wakisema maamuzi yanatakiwa kuchukuliwa.
Rwanda yaambia nchi za Ulaya zisichanganye siasa na masuala ya usalama.
Rais wa Rwanda Paul Kagame na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wakishiriki katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya - Umoja wa Afrika, mjini Brussels, Ubelgiji, Februari 17, 2022.
tokea masaa 5

Waziri wa nchi wa Rwanda Jenerali Mstaafu James Kabarebe amekutana na mjumbe maalum wa Umoja wa Ulaya (EU) kwa Ukanda wa Maziwa Makuu, Balozi Johan Borgstam, ambaye yuko katika ziara ya kikazi mjini Kigali.

Mazungumzo yao yamehusisha vikwazo ambavyo Umoja wa Ulaya umejadili kuiwekea Rwanda ikiihusisha na mzozo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

“Rwanda itaendelea kusisitiza kuwepo kwa hakikisho la usalama ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa majeshi yote ya kigeni karibu na mipaka yetu, kutatua suala la M23, na kukikataa kikundi cha FDLR,” Rwanda imesema katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo.

Umoja wa Ulaya yajadili vikwazo kwa Rwanda

Uingereza tayari imeiwekea Rwanda vikwazo ikiihusisha na waasi wa M23 wanaofanya mashambulizi DRC.

Februari 24, bunge la mataifa ya Ulaya lilijadili uwezekano wa kuiwekea Rwanda vikwazo. Wabunge walifikia makubaliano ya awali tu wakisema maamuzi yanatakiwa kuchukuliwa.

 Iwapo kutakuwa na vikwazo kutoka Umoja wa Ulaya basi itamaanisha kusitishwa kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Rwanda na EU.

Umoja huo wa Ulaya unatoa Euro milioni 20 kufadhili kikosi cha Rwanda cha kulinda amani huko Cabo Delgado, nchini Msumbiji.

Pia itamaanisha msaada wa maendeleo na makubaliano katika sekta ya madini utasitishwa
 Wakati huo huo, Marekani imemuwekea vikwazo James Kabarebe, ambaye pia ni mshauri mkuu wa masuala ya kijeshi wa rais wa Rwanda Paul Kagame, ikimhusisha na waasi wa M23.

Rwanda imeuambia Umoja wa Ulaya kuwa kanuni za uhuru wa nchi, ambazo mara nyingi zinatajwa na EU, lazima zitumike kwa Rwanda pia. Ikidai lazima itaendelea kulinda mipaka yake kutoka kwa waasi na hatari ya usalama kutoka DRC.

“ Haki za msingi za uhuru wa Rwanda zimekiukwa zaidi ya mara 20 tangu 2018 kutokana na taarifa za kupotosha. Hatua za kulinda nchi ziliwekwa kwa umakini ili kukomesha mashambulizi haya kutokea na zitaendelea kuwepo hadi vitisho hivi vitakaposhughulikiwa kikamilifu,” Rwanda imesema.

“ Inasikitisha kwamba siasa za ndani za Umoja wa Ulaya na maslahi binafsi katika eneo hilo huathiri maamuzi ya sera za kigeni za Umoja wa Ulaya badala ya EU kuzingatia ukweli. Hatua za kuadhibu ambazo zinakiuka haki za nchi hazisaidii chochote kutatua hali hiyo, katika suala hili na zinadumaza juhudi za amani zinazoongozwa na Afrika.” Rwanda imeongeza.


Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us