Afrika
3 dk kusoma
Ushirikina una nafasi gani michezoni?
Unaruhusiwa kuziita ‘ndumba’, ‘kamati za ufundi’, ‘Sangoma’, Juju na majina mengi utakavyo, lakini ukweli unabaki pale pale, kuwa kuna uhusiano wa karibu kati ya michezo na imani za kishirikina.
Ushirikina una nafasi gani michezoni?
Mashabiki wa timu ya taifa ya soka ya DRC
tokea masaa 7

Mara kwa mara, tumeshuhudia wanamichezo wakiingia viwanjani au hata ulingoni kwa mitindo tofauti. Wako wanaoingia kinyume nyume, wako wanaogusa ardhi, wapo wanaotazama juu; ili mradi kila aina ya mbwembwe, au mkwara kama wanavyoita vijana wa mjini.

 Utaratibu wa wanamichezo hawa ni maagizo kutoka kwa ‘wataalamu’, japo kuna wengine wanakuwa na mienendo ambayo hayaonekani kuwa kawaida wakiwa nje na ndani ya mchezo. Je, maagizo au matambiko yana mchango wowote katika kuwapa watu ushindi?

 Laamb ni mchezo wa mieleka uliojipatia umaarufu mkubwa katika nchi za Senegal na Gambia. Licha ya watu kushiriki mchezo huu kama sehemu ya kujifurahisha, wapo wanaoutumia mchezo huu kama sehemu ya kujipatia riziki.

Washiriki wa mchezo huu hujifunga hirizi mwili mzima. Hii ni kwa sababu wanaamini kuwa nyenzo hizo zitawasaidia kupata ushindi na kama hiyo haitoshi, waganga wao huwepo uwanjani kuhakikisha ‘ushindi unapatikana’.

 Tukija kwenye soka, mchezo maarufu zaidi na upendwao na watu wengi zaidi duniani, suala la imani za kishirikina na matambiko limekuwa jambo la kawaida kabisa.

Ni ukweli kabisa kuwa, nchi nyingi barani Afrika, iwe katika ngazi ya klabu au timu za taifa, ‘hufuata’ maagizo ya ‘kamati za ufundi’ na ‘masangoma’.

Utaratibu huu anaweza kupangiwa mchezaji maalumu, au hata wakati mwingine timu nzima, ikiwemo benchi la ufundi.

Mwaka 1974, taifa la Zaire, ambalo kwa sasa linajulikana kama DRC, lilikodi ndege maalumu kwa ajili ya ‘kamati ya ufundi’ kwenda kuisaidia timu yake ya taifa iliyokuwa inashiriki michuano ya Kombe la Dunia katika taifa lililokuwa Ujerumani Magharibi kwa wakati huo.

Katika mchezo wao kwa kwanza, ‘The Leopards’ walifungwa mabao 2-0 na Uskochi, wakifuatia na kichapo cha 9-0 kutoka kwa Yugoslavia, kabla ya kukandamizwa mabao 3-0 na Brazil.

Miaka 5 iliyopita, Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) lilipiga marufuku matumizi ya ndumba viwanjani.

Hii ni baada ya mchezaji wa Rayon Sport Moussa Camara, kukimbilia langoni mwa timu ya Mukura Victory Sports na kuondoka na kitu kisichojulikana kutoka goli la wapinzani wao, huku timu yake ikiwa nyuma kwa bao moja, na kuoneshwa kadi ya njano.

 Dakika chache baadaye, Camara aliisawazishia Rayon Sport, na hapo ndipo tabia hiyo ikapigwa marufuku nchini Rwanda.

 Mwaka 2015, Gor Mahia ya Kenya na Young Africans ya Tanzania zililaumiana kwa ushirikina wakati wa michuano ya CECAFA Kagame Cup.

Inadaiwa kuwa K’Ogalo waligoma kutumia lango kuu la Uwanja wa taifa wa Dar es Salaam wakiamini kuwa wapinzani wao walikuwa wameweka vitu fulani hapo.

Kwa upande wao, Yanga walikataa kutumia vyumba vya kubadilishia nguo kwa madai kuwa maofisa wa Gor Mahia ‘wameshafanya yao’.

 Mwaka 2022, aliyekuwa kocha wa Coastal Union ya Tanzania Melis Medo, alijiuzulu nafasi hiyo, akidai kuwa mafanikio ya timu hiyo kutoka Mkwakwani Tanga, yanarudishwa nyuma na imani za kishirikina.

Ni hivi majuzi tu,wachezaji wa Mashujaa ya Kigoma walitumia mtindo wa kuingia uwanja wa Tanganyika ‘kinyumenyume’ katika mchezo wao dhidi ya Young Africans.

 Hata hivyo, Mashujaa walichapwa mabao 5-0 katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC nchini Tanzania.

Yapo madai ya wachezaji ‘kuzindikwa kitalaamu’ au kwenda maeneo fulani usiku wa giza totoro au wengine kutakiwa kuwa uchi wa mnyama katika mazingira fulani, ili tu wapate ushindi.

Je, unadhani imani za kishirikina zina nafasi ya kuzipa timu za Afrika ushindi?

Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us